Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul- Bayt (a.s) - ABNA - Makala hii inazungumzia jinsi ya kuthibitisha Isma ya Maimamu (9) kutoka ndani ya Qur’an Tukufu. Kuna maswali mengi katika dunia hii, baadhi yake ni muhimu na mengine sio muhimu. Mengine ni ya kimantiki na mengine sio ya kimantiki. Lakini yale muhimu na ya kimantiki yanastahiki heshima ya kujibiwa tofauti na mengine yaliyobaki, na miongoni mwa maswali yanayostahiki kupewa heshima ya kujibiwa ni swali hili lisemalo:
Tunaamini kuwa watu watano (Muhammad s.a.w.w, Ali a.s, Fatima s.a, Hassan a.s, na Hussein a.s) waliokuwemo ndani ya Kisaa (kama tukio lilivyojiri katika historia) ni Maasumin.Mwenyeezi Mungu (s.w) amewatwaharisha kwa mujibu wa Aya ya 33 ya Sura ya 33, Suratul-Ahzaab.
Hivyo Isma yao hatuna shaka nayo na hakuna neno upande huo wala hakuna swali la aina yoyote ile kuhusiana na Isma yao.
Lakini wafuasi wa Ahlul-bait (a.s) yaani MASHIA ITHNA ASHARIYYA,wanaamini na kusema kuwa MAIMAM wengine tisa (9) wanaotokana na Kizazi cha Imam Hussein (a.s) nao ni Maasumina,kwamba wametwaharishwa kama wale watano wa Kisaa!.
Kwa mantiki hiyo lazima tuwaulize wale wenye kuitikadia Isma ya Maimam hao tisa (a.s), ni kwa nini mnaitikadia kuwa wao ni Maasumin na wakati hawakuwepo katika tukio la Kisaa?!, Hamuoni kuwa mnakwenda kinyume na maana mzima ya tukio lenyewe lililowahusu watano tu waliokuwepo zama hizo na sio Maimam wengine tisa waliokuja baada yao?!.
Je, mnaweza kututhibitishia kwa dalili kutoka ndani ya Qur’an au katika kauli za Mtume (s.a.w.w) kuwa wao ni Maasumina, wanayo isma?!.
Ndugu msomaji, hilo ndio swali la muulizaji, na kwa hakika ni swali la kimantiki na lina kila haki ya kuheshimiwa, na heshima yake ni kujibiwa.
Kama nilivyosema, swali hilo ni swali la kimantiki lakini jibu lake pia ni la kimantiki zaidi, na ni lenye nguvu zaidi kuliko swali lenyewe.
Tunaweza kulijibu swali hili kwa kutoa majibu mbalimbali na tofauti tofauti kulingana na ushahidi au dalili zinazopatikana ndani ya Qur’an Tukufu na katika Sunna za Bwana Mtume (s.a.w.w) juu ya Isma yao.
Binafsi nimechagua kulijibu swali hilo kwa kutumia Aya moja wapo kati ya Aya Tukufu za Mwenyeezi Mungu (s.w.t).
Na ninaanza kulijibu swali hilo kama ifuatavyo:
Mwenyeezi Mungu (s.w.t) amesema katika Suratul-Baqaraha, Aya ya 124:
“Na (Kumbukeni) Ibrahim alipojaribiwa na Mola wake kwa matamko, naye akayatimiza. Akasema: Hakika mimi nitakufanya kuwa Imam wa watu. Ibrahim akasema: Je,na Kizazi changu (pia)?.(Ndiyo,lakini) ahadi yangu haiwafikii Madhalimu.”
Hakika Aya hii Tukufu,inatosha kabisa kuthibitisha:
1: Uimam wa Maimam.
2: Isma yao (Yaani:kutotenda dhambi kwa Maimam hao,kwa ibara nyingine tunasema Aya inathibitish: Umaasum wao).
3: Pia Aya inathibitisha kuwa:Uimam hapewi mtu ambaye ni dhalimu au aliye wahi kuwa dhalimu katika uhai wake.
Na dalili yetu inasimama katika msingi huu ufuatao:
Kwanza kabisa tutambue wazi kuwa daraja ya Uimam iko juu ya daraja ya Unabii (nikisema hivyo namaanisha kwamba Uimam ni cheo kiko juu zaidi ya unabii na si zaidi ya utume),kwa maana kwamba Nabii anaweza kuwa Nabii lakini asifikie daraja ya Uimam.Hivyo Uimam ni cheo cha juu na hafikii cheo hicho yeyote ispokuwa kwa kuteuliwa au kwa kupewa cheo hicho na Mwenyeezi Mungu (s.w).
Dalili juu ya hilo nilisemalo ni Aya hiyo hapo juu ambapo Mwenyeezi Mungu (s.w) anamwambia Nabii Ibrahim kuwa:
”Hakika mimi nitakufanya kuwa Imam wa watu”.
Ndugu yangu, hebu mimi na wewe tuizingatie ibara hiyo ya Allah (s.w), anasema: “Mimi nitakufanya uwe Imam”,hajasema (watu watakufanya) uwe Imam!.
Hiyo ni nukta muhimu katika Aya hiyo, na nukta nyingine ni hii : Nabii Ibrahim (a.s) kabla ya kutangaziwa kuwa atafanywa kuwa Imam wakati huo alikuwa tayari ni Nabii, na hilo halina shaka ndani yake.Kisha baada ya kuwa sasa ashakuwa ni Nabii,Allah (s.w) anamwambia nitakuongezea cheo kingine cha Uimam uwe Imam wa watu.
Kwa muhtasari UIMAM ni cheo na ni daraja kutoka kwa Allah (s.w),haipati daraja hii ispokuwa yule aliyeteuliwa na Allah (s.w) kupitia ndimi au kauli za Manabii na Mitume wake (a.s).
Jambo la pili katia Aya hii,ni ile dua aliyoiomba Nabii Ibrahim (a.s) akikiombea kizazi chake nacho kipate daraja hiyo ya Uimam,na hiyo ni ile kauli yake pale aliposema: “Je,na kizazi changu (pia)?”.
Allah (s.w) kama kawaida yake harudisha dua ya Nabii wake yeyote yule,bali dua zao haziwekewi pazia,zinakubaliwa moja kwa moja,hivyo akakubali dua ya Nabii Ibrahim (a.s) alipokiombea kizazi chake kipate daraja hii ya juu ya Uimam,lakini Allah (s.w) hakumkumbalia kuwa kila mtu katika kizazi chake ataipata daraja hiyo bali akaweka sharti kwa atakayeweza kupata daraja hiyo kuwa lazima asiwe dhalimu,ni hiyo ni kauli yake pale aliposema: “Ahadi yangu haiwafikii madhalimu.”
*Maana ya Dhalimu: Ni mtu yeyote anayeabudia au aliyewahi kuabudia masanamu katika maisha yake (hata iwe kwa siku moja),pia dhalimu ni mtu anayetenda dhambi au aliyewahi kutenda dhambi katika maisha yake, ni mtu anayedhulumi watu au aliyewahi kuwadhulumu watu katika maisha yake,au hata kama hajawahi kuwadhulumu watu lakini kaidhulumu nafsi yake,(ameidhulumu nafsi yake) kama vile kutenda dhambi,kwa maana unapotenda dhambi unakuwa umeidhulumu nafsi yako.Kwa ufupi hiyo ndio maana ya dhalimu.
Hivyo ukiwa na moja wapo katika sifa hizo au uliwahi kuwa na moja wapo kati ya sifa hizo,basi utahesabika kuwa wewe ni dhalimu au ulisha wahi kuwa dhalimu.
Hivyo wewe kauli ya Mwenyeezi Mungu (s.w) aliposema:
“Ahadi yangu haiwafikii Madhalimu”
Itakuwa inakugusa na inakuhusu,au kwa ibara nyingine: Wewe huwezi kuupata Uimam na kuwa kiongpozi (Imam) wa watu,kwa sababu daraja hiyo ni ya wale tu ambao sio madhalimu kwa watu au kwa nafsi zao.
Hivyo hayo yote yakitubainikia wazi,kutakuwa hakuna shaka yoyote pale tutakaposema kuwa mtu atakayefikiwa na Ahadi hiyo ya Mwenyeezi Mungu (s.w) yaani (Uimam),ni lazima awe ni Maasum,yaani awe ni mtu ambaye hajawahi kutenda dhambi ya aina yoyote na wala hawezi kuthubutu kutenda dhambi ya aina yoyote ile katika maisha yake.
Huyo ndiye atakayekuwa na sifa ya kufikiwa na Ahadi ya Mwenyeezi Mungu (s.w) na kuitwa Imam wa watu kama alivyokuwa Nabii Ibrahimu (a.s) Imam wa watu baada ya Allah (s.w) kumuongezea cheo hicho na daraja hiyo ya Uimam.
Sasa ikiwa ukweli halisi wa Aya hiyo uko hivyo,basi ni akina nani katika Kizazi cha Nabii Ibrahim (a.s) waliobahatika kuwa na sifa kamili zinazotakiwa (yaani: Ambao hawajawahi kuwa madhalimu na hawatakuwa madhalimu) ili kuipata ahadi ya Mwenyeezi Mungu (s.w)?!.
Kwa hakika huwezi kuwajua wahusika wa Aya hiyo au Misdaq ya Aya hiyo au watu waliokusudiwa kuipata Ahadi ya Mwenyeezi Mungu (s.w) katika Aya hiyo ispokuwa kwa kurudi kwa yule ambaye kapewa jukumu la kuwabainishia watu yaliyoteremshwa kwao,naye ni Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Na ukirudi katika kauli za Mtume (s.a.w.w),na ukakuta popote anasema: Fulani ni Wasii wangu,au Khalifa baada yangu,au Kiongozi baada yangu, basi jua kuwa atakuwa anathibitisha Uimam wake kwa watu.
Na kitendo cha yeye (s.a.w.w) kuthibitisha Uimam wa mtu huyo,kitakuwa na mana kwamba huyo ni mmoja kati ya wale watu waliokusudiwa katika Dua ya Nabii Ibrahim (a.s) katika Aya hiyo tuliyoitaja.
Hivyo mtu yeyote ambaye itathibiti kwa kauli ya Mtume (s.a.w.w) kuwa ni IMAM baada yake,huyo atakuwa ndiye misdaq ya Aya hiyo au ndiye aliyekusudiwa kuipata ahadi ya Mwenyeezi Mungu (s.w) iliyotajwa katika Aya hiyo ya 124 ya Suratul-Baqarah,ambayo inathibitisha ISMA yake.
Na tukirudi katika kauli za Mtume (s.w),tutakutana na hadithi nyingi tu zinazothibitisha UIMAM wa Maimam watatu (3) waliokuwemo ndani ya Kisaa (na ambao tayari tukio hilo limesha thibitisha ISMA yao),na wengine tisa (9) katika kizazi cha Imam Husein (a.s) ambao ndio tunaowakusudia kuthibitisha ISMA yao sehemu hii.
Ukichukua Maimam watatu (a.s) waliokuwepo ndani ya Kisaa,ukajumlisha na Maimam wengine 9 (a.s) baada yao wanaotoka katika mgongo wa Imam Husein (a.s),utapata jumla ya Maimam kumi na wawili.Hao ndio aliotuachia Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) kuwa ndio Makhalifa baada yake na Maimam wetu na Viongozi wetu baada yake.
Hivyo tunatakiwa kuchukua kauli za Mtume (s.a.w.w) zinazo thibitisha Uimam wa Maimam hao 9, kisha tukishatambua Uimam wao,turudi katika Aya hiyo ya 124 ya Suratul-Baqarah kuthibitisha ISMA yao kama tulivyobainisha.
Hadithi za kuthibitisha Uimam wa Maimam 9 (a.s):
KUNA HADITHI NYINGI MNO ZA MTUMU (S.A.W.W) zinazothibitisha Uimam wa Maimam tisa,na hatuwezi kuzitaja zote sehemu hii bali tutataja tu hadithi moja ili kuhitimisha hoja yetu juu ya suala hili la isma yao,maana suala hilo la Uimam wao liko wazi kwa waislaam wote wenye utambuzi ispokuwa kwa wale tu Banu Umaiyya na wafuasi wa fikra zao zenye uadui wa wazi kwa Kizazi Kitukufu cha Mtume Muhammad (s.a.w.w).
HADITHI INAYOTHIBITISHA UIMAM WA MAIMA 9 (A.S):
Hadith Ithna Ashara Khalifa: (Hadithi ya Makhalifa kumi na wawili).
Muslim amepokea kutoka kwa Jabir bin Samrat, amesema:“Niliingia pamoja na baba yangu kwa Mtume (s.a.w.w), nikamsikia anasema: Kwa hakika jambo hili halikomi (haliishi, halimaliziki) mpaka wapite kwao Makhalifa kumi na wawili, amesema: (anayesema ni Jabir bin Samrat): Kisha (baada ya Mtume kuzungumza maneno hayo,) akazungumza (tena) maneno (mengine) ambayo (sikuyasikia vizuri na) sikuyaelewa, akasema (Jabir bin Samrat): Kisha nikamuuliza baba yangu: Amesema nini (Mtume hilo ambalo sikulisikia vizuri)?. (Baba yake) akasema: (Amesema hivi, hao Makhalifa kumi na wawili) wote ni katika Makuraishi”.
Tazama: Sahih Muslim: Juzuu ya 6: Ukurasa wa 3.Darul-Fikri.Bairut.
Na ametoa (au amepokea) Bukhari kutoka kwa Jabir bin Samrat, amesema:“(Mtume amesema kuwa) Watakuwa ni viongozi kumi na wawili, kisha (Mtume) akasema neno ambalo sikulisikia, baba yangu akasema (kuhusu neno hilo ambalo mimi sikufanikiwa kulisikia): Kwa hakika (Mtume) amesema hivi: Wote ni katika Maquraishi”.Tazama: Sahih Bukhari: Juzuu 8: Ukurasa wa 127.Darul-Fikri.Bairut.
Na hadithi hii ni hadithi sahihi haina shaka ndani yake kwa upande wa sanadi yake na matni yake.Wasomi maarufu wa Ahlu-Sunna kama vile Abi Ya’ala, na Twabara’niy na wengine wameinukuu hadithi hii katika vitabu vyao.
Tazama:1-Musnad Abi Ya’ala: Juzu ya 8: Ukurasa wa 444, na juzu ya 9: Ukurasa wa 222.Darul-Maamuun lit-turathi-Bairut.
1- Al-Muujamul-Kabir cha Twabara’niy: Juzu ya 10.Ukurasa wa 158.Maktabat Ibn Taimiyya-Al-qahira.
Na amesema Ahmad Muhammad Shakir kwamba: ((Sanadi yake ni sahihi)):Tazama: Musnad Ahmad, kwa Tahkiki ya Ahmad Muhammad Shakir: Juzu ya 4.Ukurasa wa 28, na 68.Na Suyutwi akasema ni “Sanadi Nzuri”.
Tazama: Tarikhul-Khulafai: Ukurasa wa 17.Darul-Maarifa.Bairut.
Hivyo basi,hadithi (hii) ni kauli ya wazi (na bayana) kwamba Makhalifa wa Mtume ni kumi na wawili, na hadithi hii inawafikiana (na kwenda sawia) na itikidadi ya Shia Imamiyya kuhusiana na Makhalifa hao kuwa ni Makhalifa kumi na wawili kutoka ndani ya Ahlul-Bait (a.s) ambao ni (Kizazi Kitukufu cha Mtume s.a.w.w ),wa kwanza wao akiwa ni Imam Ali (a.s),na wa mwisho wao akiwa ni Imam Mahdi (a.s).
Hilo likisha tuthibitikia kuwa Makhalifa {yaani:Maimam,yaani:Viongozi,yaani Mawasii wa Mtume s.a.w.w baada yake} ni kumi na wawili, watatu wakiwa ni wale wa ndani ya Kisaa,na tisa wakiwa ni wale wanaotokana na Kizazi cha Imam Husein (a.s),basi hatuna budi kurudi katika Aya yetu tuliyoitanguliza inayosema:
“Na (Kumbukeni) Ibrahim alipojaribiwa na Mola wake kwa matamko,naye akayatimiza. Akasema: Hakika mimi nitakufanya kuwa Imam wa watu.Ibrahim akasema:Je,na kizazi changu (pia)?.(Ndiyo,lakini) ahadi yangu haiwafikii Madhalimu.”
Tumetangulia kusema kuwa AHADI iliyokusudiwa katika Aya hii tukufu ni Ahadi ya UIMAM,na UIMAM huo Allah (s.w) anasema: Hauwafikii madhalimu.Na madhalimu tumetangulia kuwaelezea hapo juu kuwa ni watu wa namna gani,hivyo basi inatubainikia wazi kuwa watakao pata Ahadi hiyo ya Uimam lazima wawe ni watu wasiotenda dhambi,kwa ibara nyingine:Lazima wawe ni watu MAASUMINA, kamwe hawatendi dhambi ya aina yoyote ile,Allah (s.w) kawapa ISMA kama KINGA ya kutotenda dhambi ya aina yoyote ile.Basi ni akina nani hao waliopata AHADI hiyo?.
Jawabu nadhani litakuwa wazi na bayana kama umenisoma vizuri,waliopata ahadi hiyo tutawafahamu kupitia hadithi hiyo tuliyoitaja inayojulikana kwa jina hili: Hadith Ithna Ashara Khalifa: Yaani: Hadithi ya Makhalifa kumi na wawili, ambao wa kwanza wao ni Imam Ali (a.s) na wa Mwisho wao ni Imam Mahdi (a.t.f).
HIVYO BASI, MAIMAM TISA (9) KWA MUJIBU WA QUR’AN TUKUFU NA SUNNA TUKUFU YA BWANA MTUME (S.A.W.W) NI MAASUMIN, KAMA ILIVYOTHIBITI ISMA YA WATU WATANO WALIOINGIA NDANI YA KISAA (A.S) KATIKA TUKIO LA KISAA LILILOTHIBITI KATIKA HISTORIA SAHIHI YA KIISLAAM.
Makala hii imeandikwa na: Sheikh Taqee Zacharia Othman.
Your Comment